Mabweni shule za kata yanaweza kuzuia mimba kwa wanafunzi

Na DEOGRATIAS MUSHI

Kwa miaka ya hivi karibuni, tatizo la mimba kwa wanafunzi katika shule nyingi za sekondari za kata, na hasa zile zilizopo maeneno hya vijijini,  limekuwa moja ya maadui wakubwa wa elimu na maendeleo ya watoto wa kike.

Aidha, takwimu za Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya Tanzania wa Mwaka 2015-16  zinaonyesha kuwa, asilimia 27 ya wanawake vijana wenye umri wa miaka 15-19 tayari wana watoto au ni wajawazito tayari.

Tatizo hili lililopo karibu katika mikoa yote, linachangiwa na ukosefu wa hosteli au mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike hasa katika shule za sekondari, hali inayowafanya ama wengine kutembea umbali mrefu kwenda na kutoka shuleni huku wakikutana na vishawishi, au kuishi maisha ya kushirikiana wanafunzi wengi na kupanga katika chumba kimoja maarufu kama “gheto” ambako pia hawawi salama.

Kutokana na kulazimika kutembea umbali mrefu kwenda au kutoka shuleni, baadhi ya waendesha bodaboda wasio waadilifu, bila kujali umri wao, wameitumia hali hiyo kama chambo cha ama kuwabaka kwa nguvu, au kuwashawishi kwa zawadi ya lifti.

Utafiti wa kihabari uliofanywa katika kata za Kitunda na Kivule wilayani Ilala Mkoa wa Dar es Salaam  umebaini kuwa, licha ya juhudi kubwa za Serikali kukabiliana na tatizo hilo, tatizo bado ni kubwa.

Akijitambulisha kwa jina moja la David kutoka shule ya sekondari Misitu Kivule, anasema kuwa umbali wa shule kumepelekea matatizo mengi kwa wanafunzi hasa watoto wa kike kushindwa kukabiliana na vishawishi mabalimbali ikiwemo utoro na mimba za utoto.

Hata hivyo anaiomba sana jamii na serikali kushirikia kuweza kujenga miundo mbinu ambayo ni rafiki kwa watoto hasa usafiri ili kusaidia kuepukana na vishawishi vinavyowakabili kila siku.

Mratibu wa Elimu, Kata ya Kivule, Ulumbi Kitila, anasema juhudi za taasisi za kijamii kama Tamwa sambamba na Serikali, zinasaidia kupunguza tatizo hilo ikilinganishwa na hali ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.

“Hii inatokana na elimu kutolewa bure kwa watoto wa shule zote zikiwemo 9 za sekondari na 10 za msingi katika kata hii ya Kivule. Hii imechangiwa zaidi na uwepo klabu za watoto zilizoanzishwa ili kutoa elimu kuhusu madhara ya mimba kwa watoto wa shule na namna sahihi ya kuziepuka.”

Anasema elimu ya afya hutolewa shuleni kwa makundi rika kwa kuzingatia umri na somo linalofundishwa.Lingine muhimu linalosaidia kupunguza tatizo la mimba kwa wanafunzi, anasema ni utaratibu waliojiwekea wa kukutana na wazazi kuwahimiza umuhimu wa kuwa karibu na watoto.

Tatizo hili linashamiri kwani baadhi ya wasichana wanapofaulu katika elimu ya msingi, hupangiwa shule zilizo mbali hali inayowafanya wakutane na vishawishi njiani, hatari ya kubakwa au kushambuliwa, wengine hata kuishi katika nyumba gheto moja wavulana na wasichana ili wachangie gharama za maisha kwa kodi ya nyumba na mahitaji muhimu kama chakula.

Kiongozi huyo anadai kuwa katika eneo lake hakuna takwimu zinazoonesha kuwepo kwa wanafunzi walioachishwa masomo na kuolewa au kupata ujauzito, hali anayosema ni ya kujivunia.

“Kwa sasa kila kata kuna polisi ambao moja ya majukumu yao ni kusaidia kudhibiti utoro miongoni mwa watoto,” anasema Kitila, na kuongeza kwamba hatua hiyo inaweza kuwa moja ya sababu zilizopunguza tatizo hilo.

Lakini pia anasema kamati za shule zimeagizwa kukutana mara nne kwa mwaka kujadili maendeleo ya shule ikiwa ni pamoja na kudhibiti utoro.

“Katika vikao hivyo vya shule wazazi wanakubaliana kutoa lishe kwa wanafunzi hatua ambayo imesaidia kupunguza utoro,” anasema.

Mmoja wa walimu katika Shule ya Msingi Kivule ambaye hakutaka jina jina lake litajwe anasema tatizo la mimba kwa wanafunzi huchangiwa pia na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi. Anasema awali, hali hiyo ilichangiwa na uelewa mdogo miongoni mwa watu kuwa, kumpatia mtoto elimu ya afya ya uzazi, ni sawa na kumruhusu kufanya ngono.

“Hii imechochea kasi ya mimba za utotoni na zinazofifisha ndoto za wasichana wengi wanaojikuta wanakatisha masomo na kulea watoto wao huku nao wakiwa bado watoto bila kutarajia,” anaeleza.

Mwalimu huyo anaamini ni jambo la kujivunia kuwa, Serikali imejipanga kuhakikisha wanafunzi wakike hawakatizwi ndoto zao kwa kupata ujauzito.

Mwalimu huyo anadai changamoto kubwa ni kwa wanafunzi wa kike  hususan waishio vijijini ambao hawajafikiwa na huduma ya elimu ya afya  inatoyolewa  shuleni kwa makundi rika kwani inasaidia kupunguza mimba kwa wanafunzi wa kike.

“Ili wanafunzi wa kike waweze kufikia malengo yao, Serikali inatakiwa kutokomeza mazingira hatarishi yanayosababisha mimba za utotoni,” anasisitiza.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia wa Tamwa katika Kata ya Kivule, Zahara Mzee, anasema matukio ya watoto kupata ujauzito yapo katika kata hiyo ingawa mengi huwa hayafiki mbali kutokana na wazazi kumalizana kienyeji na watuhumiwa.

Anasema tamaa ya mali na kuwageuza watoto wa kike kama mitaji ya familia, uhaba wa mabweni kwa ajili ya wasichana pamoja na baadhi ya tamaduni, ni miongoni vichocheo na visababishi vya mimba shuleni.

Lilian Mohamed (sio jina halisi), ni mmoja wa watoto aliyepata mimba akiwa kidato cha tatu na kujikuta njiapanda baada ya kijana aliyemsababishia ujauzito huo, kumkana mbele ya wazazi wake Lilian akisema hahusiki na ujauzito huo.

Mwenyewe anasema, ndoto zake kimaisha zimeingia doa kwani hata wazazi wake wanaonesha wazi dalili za kumsusa japo, baada ya tukio hilo aliwaomba msamaha kwani alishawishiwa ili kupata nafuu ya usafiri kwenda shuleni kwa kutumia lifti ya bodaboda.

Mwanafunzi mwingine wa Kidato cha Tatu  katika Shule ya Sekondari ya Kitunda wilayani Iala anasema hivi:  “Tungekuwa tuna mabweni katika shule zote, vishawishi wasichana vingepungua maana tungekuwa tunajisomea bweni au ku-discuss (kujadili) pamoja tukienda prep. (masomo ya kujiandaa), lakini wakati mwingine hasa mitihani ikikaribia inabidi utoke nyumbani kwenda kudiscuss huko nako saa nyingine hata wanafunzi mnaacha ku-discuss mnaanza kujadili mengine…” anasema Sakina.

Anaongeza: “Hawa bodaboda wakijua unatoka mbali wanakuwa wanakufuatafuata wanakwambia wanakupa lifti unakataa wanalazimisha mwisho unaona labda wanataka kukusaidia usichelewe kipindi, baadaye mtu anakugeuzia kibao ili eti awe anakuwahisha shule au nyumbani kila siku.”

Mmoja wa waendesha bodaboda, aliyejitambulisha kuwa mkazi wa Matembele- Kivule anapinga madai kuwa, bodaboda huwarubuni wanafunzi wa kike na kuwakatisha masomo kwa mimba. “Hiyo inaeza kuwa ni tabia ya mtu mmoja mmoja sio wote,” anasema Said Ghati.

Mgaya Nyangige, mzazi wa mwanafunzi wa kike katika darasa la tatu shuleni hapo anasema, “Shule za kulala (anamaanisha bweni), ni muhimu maana mtoto anatoka shule au nyumbani, lakini hapo katikati kuna mambo mengine anakutana nayo njiani ndiyo maana wengine wanapata mimba. Kila shule ikiwa ya kulala huko, hata watoto wa kike watashinda vizuri.”

Hata hivyo, watu mbalimbali wakiwamo walimu, wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia wanasema, mimba za utotoni shuleni, ni tatizo kubwa ingawa matukio mengi hayaripotiwi katika mamlaka husika na mengine, wahusika kuficha au kukwepa kutoa ushahidi wa kuwatia hatiani wahusika.

Kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (Sospa) ya Mwaka 1998, mwanaume yeyote anachukuliwa kuwa amebaka endapo pia atajamiana kwa ridhaa, au bila ridhaa na msichana mwenye umri chini ya miaka 18, au mwanafunzi wa shule.

Wengi, wanaulaumu utaratibu unaotumika mara nyingi kuwa, endapo mtoto atakaa siku 60 mpaka siku 75 bila kuhudhuria masomo, basi shule humchukulia kama mtoro na kuwa amejiondoa mwenyewe masomoni na kwamba, hali hiyo pia ni kikwazo katika vita dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.

Inapendekezwa kuwa, wazazi waimarishe tabia ya kutoficha endapo watoto wao wanakutwa na ujauzito kwani baadhi ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne wengine hukaa miezi michache na kujifungua, hali hiyo inaonesha kuwa, wakati akifanaya mtihani alikuwa mjamzito.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Salum Hamduni, anasema matukio ya mimba shuleni mengi hayaripotiwi katika vituo vya polisi, hivyo  ni changamoto kujua makosa hayo na kuiomba jamii kuacha kumalizana nyumbani na kuripoti matukio hayo katika vyombo vya sheria.

Hata hivyo, licha ya kukosekana kwa takwimu halisi za tatizo katika maeneo ya kivule, ukweli unabaki palepale kuwa, ndoa za mapema na mimba za utotoni hususani kwa wanafunzi, ni tatizo kubwa la kijamii linalohitaji nguvu ya pamoja tangu ya wanajamii, viongozi wa dini, wanasiasa, pamoja na watunga sera na sheria ili kukabiliana nalo.

 

mwisho