TGNP Mtandao yakutanisha wadau kujadili Tanzania ya viwanda na wanawake.

Na Joachim Mushi

TGNP Mtandao imekutanisha wajumbe kutoka makundi mbalimbali ya wadau wa maendeleo wakiwemo wawakilishi kutoka taasisi za umma na Serikali , asasi za kiraia na wadau wa maendeleo kujadili uchambuzi uliofanywa na taasisi hiyo kuangalia sera, mikakati na mipango ya Serikali kumuwezesha mwanamke kuelekea uchumi wa viwanda.

Akizungumza wakati akifungua majadiliano, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Lilian Liundi leo jijini Dar es Salaam amesema taasisi hiyo imefanya uchambuzi wa sera, mikakati na mipango ya Serikali kuangalia ushiriki wa wanawake na makundi mengine ya pembezoni katika Tanzania ya viwanda.

Alisema katika uchambuzi huo uliofanywa kushirikiana na  Profesa Flora Kessy, Mtaalam wa uchambuzi wa sera umeangalia maeneo mbalimbali ikiwemo changamoto za kundi la wanawake linavyoweza kushirikishwa kwa mafanikio ya Tanzania ya viwanda.

Mkurugenzi Mtendaji TGNP Mtandao, Lilian Liundi akifungua mjadala huo. 

Akifafanua zaidi, Bi. Liundi aliwataka wajumbe hao kujadiliana kwa kuzingatia kuwa takwimu za ‘UN Women’ zinaonesha mwanamke ni uti wa mgongo wa maendeleo kutokana na kuchangia takriban kwa asilimia 43 katika nguvu kazi duniani na kwa nchi nyingine asilimia hiyo inafikia hadi 70.

Alisema kwa upande wa Tanzania kilimo kinaajiri zaidi ya asilimia 65.5 ya Watanzania huku idadi kubwa ya kundi hilo wakiwa ni akinamama, jambo ambalo linaonesha upo umuhimu mkubwa wa kundi hilo kuangaliwa kipekee katika uwezeshwaji kufikia malengo kuelekea uchumi wa viwanda.

Hata hivyo alisema bado kuna changamoto nyingi katika kundi la wanawake kuelekea uchumi wa viwanda, ukizingatia kundi kubwa la wanawake liko katika sekta isiyo rasmi (asilimia 51.1), idadi ndogo ya wanawake wanaomiliki ardhi (asilimia 8) ukilinganisha na wanaume, idadi kubwa ya wanawake kuwa katika kundi la umasikini (asilimia 60) ukilinganisha na wanaume.

“…Jinsia ni suala la Maendeleo hatuna budi kwa pamoja kutoa kipaumbele ili kuongeza ushiriki wa wanawake wenye tija katika maendeleo ya uchumi wa nchi. Ni wazi kuwa mkutano huu utatumika kujadili kwa kina na kupanga mikakati ya kuimarisha ushiriki wa wanawake pamoja na sera hizo bado kuna changamoto ya utekelezaji ili kuwezesha ushiriki wenye tija kwa wanawake na makundi ya pembezoni,” alisema Bi. Liundi.

“Katika kusisitiza ushiriki wa Wanawake katika Tanzania ya Viwanda tuzingatie kanuni (principle) ya malengo endelevu ya dunia ya kutomwacha mtu nyuma kwa kufanya uchambuzi wa kina kwa jicho la jinsia ili kuleta ushiriki jumuishi na wenye tija. Ikumbukwe kwamba tukiacha kundi la wanawake nyuma tunapoteza fursa na mapato kwa kiasi kikubwa hivyo kutuchelewesha kufikia uchumi wa kati na dira yetu ya 2025,” alisema.

Kwa upande wake  Prof. Kessy akiwasilisha uchambuzi kwa washiriki hao alibainisha kuwa shughuli wanazozifanya akinamama kwa sasa zinaweza kuboreshwa zaidi kulingana na mahitaji hivyo kujikuta kundi hilo linajengewa uwezo.

Alisema shughuli kama uzalishaji mdogo mdogo unaofanywa na kundi hilo unaweza kuongezewa teknolojia, masoko pamoja na nguvu za uzalishaji na kukuta inamuinua mwanamke na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa viwanda.

Kundi hilo kwa pamoja litajadili na kuchakata changamoto hizo na kutoka na mapendekezo ambayo watajaribu kuishirikisha Serikali kupitia wizara husika ili kuona uwezekano wa kuzingatiwa kwa mapendekezo ya wadau hao.

Washiriki kutoka taasisi za raia na serikali pamoja na wadau wa maendeleo wakijadali uchambuzi huo