Masuala ya Kijinsia yahitajika kwenye mitaala ya elimu za msingi na sekondari Tanzania.

Dar es Salaam. Wanaharakati wa haki za watoto na wanawake nchini wamepewa changamoto ya kuandaa mapendekezo yatakayowezesha kuwapo kwa mitaala ya kupinga ukatili wa kijinsia itakayowasaidia watoto kupewa elimu ya kupambana na suala hilo tangu wakiwa shule za msingi.

Takwimu za ukatili wa kijinsia  nchini zinaonyesha kati ya watoto wakike watatu mmoja ameshafanyiwa ukatili wa kingono, wakati kati ya watoto saba wa kiume, mmoja amefanyiwa ukatili huo.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika viwanja vya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) likiwahusisha wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori alisema takwimu za ukatili wa kijinsia zilizopo zinatisha na kwamba inahitaji nguvu ya pamoja kupambana nazo.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori akizungumza katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili TGNP Mtandao

Makori alisema kwa muda mrefu wanaharakati wamekuwa wakipambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia lakini bado yapo matukio yanayoendelea kyutokea kwenye jamii.

Alisema lazima ipatikane dawa ya kupambana nayo moja wapo ikiwa mitaala itakayotumika kuwafundisha watoto hao namna ya kujilinda tangu wakiwa wadogo.

 “Bado mnayo kazi moja kwenye mapambano haya, fanyeni utafiti na kuandaa mapendekezo ya namna gani tutaandaa mitaala ya kuwasaidia watoto wetu kuwa na uelewa wa masuala haya tangu wakiwa wadogo. Lazima tutokomeze huu ukatili,”alisema  Makori.

Kaimu Mkurugenzi wa TGNP, Grace Kisetu alisema ni kweli kwamba ukatili wa kijinsia ni vita inayohitaji nguvu ya pamoja kupambana nayo.

Kaimu Mkurugenzi wa TGNP, Grace Kisetu akizungumza katika maadhimisho hayo

Alisema maadhimisho ya mwaka huu wamewahusisha wanafunzi wa shule za msingi, Sekondari na vyuo vikuu kwa sababu ni kundi maalum linalopaswa kuelewa na kujua namna ya kujikinga wakati wanapokutana na ukatili huo.

Alisema kimsingi kiwango cha ukatili huo nchini ni kikubwa na kwa mujibu wa taarifa za Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Maralia ya 2015/2016 wanawake wanne kati ya 10, wamewahi kufanyiwa ukatili wa kwimwili tangu wakiwa wadogo.

Alisema katika maadhimisho hayo wamefanya utafiti shirikishi kwenye shule za msingi na sekondari za jijini Dar es Salaam na kubaini bado zipo changamoto nyingi zinazochochea kuwapo kwa ukatili huo.

Alitaja changamoto hizo kuwa baadhi ya watoto kuishi mbali na ziliko shule na hivyo kukutana na ukatili wa kijinsia ikiwamo kubakwa wakati wa kwenda na kurudi shule.

Mwalimu wa shule ya msingi Kilimani, Jagita Malyango alisema wamefanikiwa kuanzisha klabu ya jinsia shuleni kwao inayosaidia katika kupambana na yukatili wa kijinsia.

“Tangu tumeanzisha hizi klabu shuleni, watoto wengi wanaweza kueleza ukatili wanaokumbana nao majumbani, njiani hata wakiwa shuleni na tunaweza kuwasaidia. Kwabla ya mitaala, ni vizuri ziundwe klabu za jinsia,”alisema.

Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kutoka wilaya za Kinondoni, Temeke na Ubungo wakiwasilisha maswala yalioibuliwa katika tafiti shirikishi zilizofanywa mashuleni kwao. 

Mwisho.