TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI: YALIYOJIRI TAMASHA LA JINSIA 2017.

{:en}

YALIYOJIRI KWENYE TAMASHA LA JINSIA LA 14, 2017

MADA: Mageuzi ya mifumo kandamizi kwa usawa wa kijinsia na Maendeleo Endelevu”

Tamasha la Jinsia la 14 linahitimishwa leo, Tarehe 8 Septemba 2017, baada ya siku nne za sherehe, tafakuri, mijadala na pongezi. Tamasha lilizinduliwa kwa hotuba ya kusisimua na yenye busara nyingi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan. Pia, Makamu wa Rais alijumuika nasi katika kuwatambua, kuwasherehekea na kuwaenzi  wanawake walioonyesha ujasiri katika Harakati za Ukombozi wa Mwanamke Kimapinduzi, na Halmashauri za Wilaya za Kishapu na Kisarawe ambazo zimefanya vizuri katika kuingiza masuala ya kijinsia katika bajeti za halmashauri zao. Wanawake waliopata tuzo ni pamoja na Mhe. Makamu wa Rais mwenyewe, Mhe.   Mama Getrude Mongella, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Anna Makinda, Profesa Daktari Mama Esther Mwaikambo, Mhe. Mama Anna Abdalla na Mhe.  Dada Esther Bulaya, Mbunge Bunda Mjini. Wengine ni  Wanachama wa TGNP  Mtandao  waliotoa mchango mkubwa  katika kujenga  Tapo  la Ukombozi  wa wanawake  kimapinduzi akiwemo  Dada  Profesa Marjorie Mbilinyi, Asseny Muro, Mary Rusimbi, Demere Kitunga, Subira Kibiga , Aggripina Mosha na   Zippora Shekilango

Tamasha la mwaka huu, limehudhuriwa na washiriki zaidi ya 1500 wakiwakilisha AZAKI mbalimbali, Vikundi vya kijamii, Serikali, Taasisi za Elimu ya Juu, Wadau wa Maendeleo, Taasisi za Vijana, vyama vya siasa, viongozi mbalimbali na watu binafsi kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.

Katika Tamasha, siku ya pili na ya tatu kumekuwa na warsha mbalimbali (nane) na mijadala ya kina juu ya haki ya kiuchumi kwa wanawake na rasilimali kuwanufaisha wanawake na wanaume walioko pembezoni. Pia tumejadili uwekezaji wa rasilimali ili kuendeleza usawa wa kijinsia, upatikanaji wa huduma za jamii, na ukatili wa kijinsia  na namna unavyoathiri ushiriki wa wanawake katika maendeleo. Kulikuwa na ushiriki mkubwa wa kimkakati wa vijana hususan wa kike ili kukuza mijadala kati ya rika moja na lingine.

Katika warsha na mijadala hiyo, washiriki waliibua masuala kadhaa na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike ili kupata suluhisho la changamoto na vikwazo kwa wananchi.  Kwa Ujumla washiriki  waliona  kuwa pamoja na kutambua na kusherehekea mafanikio  ya ushiriki uliotukuka wa wanawake katika michakato mbalimbali ya kuleta usawa wa jinsia na Maendeleo, bado kuna changamoto  hususan za kimifumo ambazo  zinaminya  fursa za wanawake  kushiriki kikamilifu  katika Maendeleo. Mifumo ya Kiunchumi bado haijaweza kumkomboa  mwanamke hasa wale masikini na wa vijijini. Mifumo ya kisiasa nayo bado ina changamoto katika kutoa fursa sawa za ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi  katika nyanja zote. Zaidi mifumo ya kijamii  hususan ufikiaji wa huduma za kijamii bado inazidi kuwaongezea wanawake mzigo wa majukumu huku wakisukumwa  kwa kiasi kikubwa katika sekta isiyo rasmi.

Yafuatayo ni baadhi ya masuala yaliyoibuliwa:

 1. Utengwaji wa rasilimali bado ni changamoto hasa katika kukuza na kuendeleza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake. Kwa mfano, ni asilimia 20 tu ya wanawake Tanzania wanamiliki ardhi. Kumekuwa na ufinyu wa rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya asasi za kiraia na vikundi vya kijamii hasa hasa rasilimali fedha, ujuzi, teknolojia na taarifa sahihi. Na hii imesababishwa na utegemezi kwa wafadhili kwa kiwango kikubwa. Kwa upande wa serikali, licha ya juhudi zinazofanyika, ikiwemo kutenga asilimia 10 ya fedha za serikali za mitaa kwa ajili ya wanawake na vijana, bado kuna changamoto ya taarifa sahihi juu ya nani ananufaika nazo na nini kifanyike kuboresha hali hiyo. Aidha, hakuna mfumo mzuri wenye uwazi na endelevu wa ufuatiliaji wa rasilimali na utoaji wa mrejesho.
 2. Mfumo wa kukusanya takwimu, kama vile za umiliki wa ardhi, una mapungufu mengi. Zoezi hili linatakiwa kufanyika kwa umakini zaidi ili kuonesha mgawanyo wa umiliki wa ardhi wa wanawake, ukatili wa kijinsia na mimba za utotoni – ili lisaidie katika kutatua changamoto.
 3. Uwekezaji katika sekta ya kilimo – wa pembejeo, maafisa ugani, masoko – uende sambamba na hali halisi ya uzalishaji ili kuboresha maisha ya wananchi na kuchangia ipasavyo katika Tanzania ya viwanda.
 4. Sera mbalimbali za kumwezesha mwanamke na kuinua usawa wa kijinsia haziendani na mazingira ya sasa. Kwa mfano, mitaala ya elimu iliyopo haiendani na sera ya kuelekeza Tanzania kwenye viwanda na uchumi wa kati. Sera zifanyiwe marejeo ili ziendane na muktadha wa sasa, na ziwe na mrengo wa kijinsia. Pia, ziendane na miongozo na mikakati mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kama vile malengo ya maendeleo endelevu, Ajenda ya Afrika 2063, Mkataba wa Jinsia na Maendeleo wa SADC, mpango wa maendeleo wa miaka mitano na mpango wa taifa wa kutokomeza ukatili wa kijinsia.
 5. Bajeti kuu na bajeti za serikali za mitaa zizingatie mahitaji ya kijinsia kwa makundi yote. Bajeti iwe ya kutekelezeka, itolewe kwa wakati na kwa kiwango kilichopangwa. Vile vile, mchakato wa kuandaa bajeti uwe shirikishi na wa uwazi, bila kujali tofauti za kijiografia, rika, hali ya uchumi, jinsi, elimu na hali ya ulemavu. Washiriki wa Tamasha tumeazimia kuweka nguvu za pamoja katika kufanya uchambuzi na kufuatilia mchakato wa bajeti na kutoa mrejesho na mapendekezo ya kuboresha mipango na bajeti za serikali katika  ngazi ya Jamii  hadi taifa.
 6. Tanzania ya viwanda na kuelekea uchumi wa kati inahitaji nguvu kazi yenye afya bora na weledi. Hivyo basi, mikakati ya kupunguza vifo vya kina mama na watoto ni muhimu. Hivi sasa watoto 67 kati ya vizazi hai 1,000, na wanawake 556 kati ya 100,000 wanakufa kutokana na huduma duni za afya ya uzazi. Bajeti ya afya iongezwe kufikia asilimia 15 ya bajeti ya taifa, kama  Azimio la Abuja linavyotamka. Pia wananchi watambue wanajukumu  la kufuatilia na kutoa taarifa za vifo na kudai uwajibikaji kwa wahusika.
 7. Upatikanaji wa maji safi na salama bado ni changamoto kubwa, wanawake bado wanatembea kati ya saa tatu hadi tano kutafuta maji. Pia, ukosefu wa maji shuleni na katika vituo vya afya  na zahanati ni changamoto nzito sana. Hii husababisha wanawake wajawazito kubeba ndoo za maji wakati wa kwenda kujifungua, na watoto wa kike kukosa masomo ya siku 40 hadi 50 kwa mwaka wakati wa hedhi. Hivyo, wanafunzi hao hukosa haki yao ya msingi ya masomo na kufaulu vizuri.  Vile vile, maendeleo ya viwanda yatahitaji maji zaidi ili kuwezesha uzalishaji.  Haya yote yataongeza mahitaji ya maji kwa kiwango kikubwa, na hivyo kusababisha ushindani wa uhitaji wa maji kati ya binadamu, mifugo na viwanda, ambapo waathirika wakuu watakuwa ni wanawake.
 8. Mimba za utotoni zimeendelea kuwa changamoto na kikwazo kikubwa sana cha wasichana kupata haki yao ya elimu. Kwa mujibu wa Idara ya Maendeleo ya Vijana – Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, mimba za utotoni nchini zimeongezeka kutoka asilimia 23 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 27 mwaka 2016/17, kutokana na ukosefu wa huduma ikiwemo  elimu ya afya ya uzazi kwa vijana wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 19.
 9. Kuna mapungufu makubwa katika utunzanji wa kumbukumbu, hasa za wanawake wanaochangia katika maendeleo ya taifa, licha ya kwamba wanawake wanachangia maendeleo bega kwa bega na wanaume lakini kumbukumbu zao hazijaandikwa. Na ndio maana katika Tamasha hili, kufuatia utafiti wetu mdogo, TGNP ILITOA TUZO kwa baadhi ya wanawake hao kama sehemu ya kutambua michango yao, na sehemu ya mipango endelevu ya kurithisha ujuzi na maarifa kwa vizazi vipya pamoja na kujifunza kwa wanawake na wanaume waliobobea katika nyanja maalum.

Mikakati

 • Kushirikisha wadau mbalimbli zikiwemo AZAKI, wadau wa maendeleo, asasi za elimu ya juu na taasisi za serikali katika kutafuta na kufanya uchambuzi ili kupata taarifa na takwimu sahihi juu ya mimba na ndoa za utotoni, ukatili wa kijinsia  na umiliki wa ardhi kwa wanawake na watu wenye ulemavu.
 • Kuendelea kuimarisha mikakati ya kuweka kumbukumbu za wanawake waliotoa michango katika maendeleo kwenye nyanja mbalimbali na kuzisambaza taarifa za kumbukumbu hizo kwa ajili ya watu kujifunza na kuwaenzi wanawake hao. Pia, kupanua wigo wa kutoa mafunzo ya kimwongozo katika kuchukua na kuhifadhi kumbukumbu za wanawake kwa AZAKI, vijana na wadau wengine.
 • Kuweka mipango endelevu ya kurithisha ujuzi na maarifa kutoka kizazi/rika moja kwenda nyingine, hasa kutoka kwa wanawake waliobobea kwenye tasnia mbalimbali.
 • Zaidi ya 60% ya Watanzania wakiwa vijana, sera na mipango iingize masuala ya vijana ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo katika nyanja zote. Pia, rasilimali za kutosha zitengwe ili kuwezesha utekelezwaji wa mipango na mikakati ya vijana bila kujali itikadi, jinsi, dini, jiografia na hali ya kipato.

{:}{:ru}

{:}