TGNP Mtandao imetoa tuzo kwa wanawake katika Nyanja na ngazi mbalimbali ikiwa ni sehemu ya ishara ya kuonesha kujali na kutathimini michangao yao.

Akizungumza wakati wa shughuli ya kukabidhi tuzo hizo iliyofanywa na Mhe. Samia Suluhu, Makamu wa Rais, Dr. Vincesia Shule, Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Mtandao amesema wanawake wamekuwa chanzo cha mafanikio ya watu binafsi, taasisi mbalimbali na taifa kwa ujumla.

“TGNP Mtandao kwa kushirikiana na Kamati ya Taifa ya Uwekezaji wa Kumbukumbu za wanawake nchini, kwa miaka mingi imekuwa ikiweka kumbukumbu za michango mbalimbali kwa kufanya tafiti juu ya maisha ya baadhi ya wanawake, kuandika hadithi za maisha yao na kuweka taarifa hizi katika tungo, picha , michoro na vitabu,” amesema  Shule.

Wanawake waliopewa tuzo ni wanachama wa TGNP, Fides Chale (hayati), Prof. Marjorie Mbilinyi, Agripina Mosha, Mary Rusimbi, Demere Kitunga, Aseny Muro, Zippora Shekilango na Subira Kibiga n.k.

[huge_it_slider id=”2″]

Pia wamo Samia Suluhu, Makamo wa Raisi Theresia Mahagatila ( dereva  wa treni wa kwanza nchini), Esther Bulaya, Mbunge wa jimbo la Bunda kwa jitihada zake za kupambana na mfumo dume katika nafasi za uongozi, Mwami Theresa Ntare wa IV (Mwanamke wa kwanza mwenyekiti wa baraza la machifu Tanzania) na Pili Hussein (mjomba Hussein) –mchimbaji wa kwanza  mwanamke nchini.

Wengine ni Anna Makinda- Spika wa kwanza mwanamke wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Getrude Mongela ambaye ametoa mchango katika harakati za kusimamia na kupigania usawa wa kijinsia ndani na nje ya nchi, Anna Abdallah , Asha Rose Migiro, Thabitha Siwale, Ester Mwaikambo-dakatari wa kwanza mwanamke, Florah Mathias –mwanaharakati ngazi ya jamii na Fatuma Binti Baraka (hayati Bi. Kidude) ambaye alifanya harakati za ukombozi wa wanawake kwa kutumia muziki wa taarabu.