Makamu wa Rais azindua tamasha la jinsia 2017

Mhe. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, leo amezindua rasmi tamasha la jinsia la 14 huku akisisitiza kuwa “ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi na uongozi ni suala muhimu katika kuhakikisha nchi inapata maendeleo na kufikia usawa wa jinsia.”

Akizindua tamasha hilo katika viwanja vya TGNP-Mtandao vilivyopo Mabibo jijini Dar es Salaa Suluhu, amesema uwezeshaji wanawake kiuchumi ni nyenzo muhimu katika kukuza usawa wa kijinsia na kuwezesha Tanzania kufikia azma yake ya kufikia uchumi wa kati unaoendeshwa na viwanda.

“Kwa kuzingatia hilo, serikali imechukua hatua mbalimbaliu ili kumwezesha mwanamke kujikomboa kiuchumi. Hatua hizo ni: kuanzisha Benki ya Wanawake Tanzania; kuanzisha mifuko mbalimbali ya uwezeshaji ukiwemo mfuko wa Maendeleo ya Wanawake pamoja na kuhamasisha uanzishwaji wa SACCOS na VICOBA,” amesema Suluhu.

Aidha, serikali iliagiza asilimia 30 ya zabuni za serikali zipewe wanawake wenye uwezo na halmashauri zote kutenga asilimia tano ya mapato yao kwa ajili mfuko wa maendeleo ya wanawake.

Mhe. Samia Hassan Suluhu, Makamu wa Raisi akizindua Tamasha la Jinsia 2017

Suluhu amesema ili kufikiwa usawa wa kijinsia lazima mwanamke na mtoto wa kike wapewe mbinu za kuwawezesha kiuchumi na kulindwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

“Pamoja na jitihada hizi takwimu za Jeshi la Polisi zinaonesha kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake  na watoto vinaendelea kutokea hapa nchini. Katika kukabiliana na hali hiyo, serikali imeandaa mpango wa Taifa wa miaka mitano wa kutokomeza ukatili dhidi  ya Wanawake na watoto,” amesema Suluhu.

Mpango huo wa miaka mitano uliozinduliwa Disemba, 2016 na utekelezaji wake kuanza mwaka 2016/2017 unalenga kuzuia na kukabiliana na vitendo vya ukatili.

Aidha, Aidha, Lilian Liundi, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao amesema tamasha la mwaka huu limeandaliwa na Azaki mbalimbali zaidi ya 100 na kuongozwa na TGNP ambapo mada kuu ni “mageuzi ya mifumo kandamizi kwa usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu”

“Mbali na lengo kuu, lakini pia tamasha lina malengo mahususi ya: kutafakari na kusherekea mafanikio, kujadili changamoto na kuweka mikakati ya pamaoja kutatua changamoto hizo, kutathmini ushiriki wa wanawake katika michakato ya kufanya maamuzi na ngazi ya uongoz,” amesema Liundi.

Liundi ameongeza kuwa malengo mengine ni “kufuatilia, kuhifadhi, kutambua na kusherehekea viongzi wanawake wenye michango ya kuigwa juu ya usawa wa kijinia na uwezo wa wanawake hususani mapambano dhidi ya mifumo dume na kuimarisha harakati na nguvu za pamoja katika ukombozi wa mwanamke.