Tamko la TGNP Mtandao kuhusu ripoti za uchunguzi wa mchanga wa madini (Makinikia)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MIFUMO YA KISHERIA IBORESHWE KUEPUSHA UPORAJI WA RASILIMALI ZA TAIFA

 

TGNP Mtandao tumekuwa tukifuatilia kwa ukaribu hatua kwa hatua namna ambavyo Serikali inashughulikia suala la kulinda rasilimali za umma ili ziwanufaishe watanzania wote. Tumefuatilia ripoti za Tume mbili za Rais ambazo zilikuwa zikichunguza suala la usafirishaji nje mchanga wa madini (makinikia), ambazo zote zimeshawasilishwa kwa Rais na kuonyesha nchi yetu imekuwa ikipoteza mabilioni ya fedha kwa uzembe ambao ungeweza kudhibitiwa.

 

Tangu mwaka 1998, TGNP Mtandao kushirikiana na Muungano wa Mashirika Watetetezi wa haki za Binadamu, Demokrasia, Utawala Bora na Usawa wa Kijinsia, (FemAct), tumekuwa tukipaaza sauti kupitia kampeni yetu ya Rudisha Rasilimali kwa Wananchi” kutoa wito kwa serikali ili ichukue hatua  kulinda rasilimali za umma kama madini, misitu, wanyama pori na nyingine. Lakini kwa bahati mbaya nchi yetu haikuwa na sheria thabiti na mifumo ya kulinda rasilimali hizi na kusababisha uporaji mkubwa ambao umetufikisha hapa.

 

Hatua iliyochukuliwa na Mh. Rais John Pombe Magufuli ni hatua ya kizalendo na ishara nzuri kwetu sisi, na kwa wananchi hususan wanawake na wanaume walioko pembezoni na huu ni mwelekeo wa mafanikio ya kampeni yetu hiyo.

Ni jambo lisilopingika kwamba kumekuwa na changamoto kubwa katika upatikanaji wa huduma bora za jamii kama maji, elimu na afya hasa afya ya uzazi ambapo mwanawake na mtoto amekuwa mwaathirika mkubwa kwa ukosefu wa huduma hizi. Katika uchambuzi wa sera, mipango na bajeti ya taifa kwa mtazamo wa kijinsia inaonesha utengwaji wa kiasi kisichokidhi kuboresha upatikanaji wa huduma bora za jamii ambazo ni chachu kubwa katika  maendeleo jumuishi.

Ushauri wetu kwa Mhe. Rais ni kuweka misingi imara ya kimfumo ikiwepo, marekebisho ya sheria zote za madini, Petroli na Gesi ambazo baadhi zilipitishwa kwa hati za dharura huko nyuma na kuyapa makampuni binafsi mwanya wa kupora rasilimali zetu. Mfano kifungu cha 25 (1) cha sheria ya madini namba 14 ya mwaka 2010, kinaeleza kwamba ripoti inayohusu masuala ya madini ni siri ya mmiliki wa hati miliki ya mgodi.  Kusingekuwepo na sheria hii kandamizi yenye  usiri udanganyifu kama uliojitokeza kwenye taarifa za makontena ya mchanga wa madini zaidi ya 200 bandarini usingetokea.

 

Kwa mantiki hiyo, tunaitaka serikali kufanya yafuatayo ili taifa letu lisiingie tena katika tatizo kama hili: –

 

  • Kuifanyia marekebisho sheria   ya uwekezaji Tanzania ya mwaka 1997, ambayo inawapa wawekezaji wa kigeni ulinzi mkubwa na manufaa mengi kama vile kutoa nje ya nchi  fedha na faida yote wanayopata kwa uwekezaji wao nchini. pamoja na sheria ya madini  namba 14 ya mwaka 2010, ambazo zinampa mamlaka makubwa mwekezaji kwenye sekta ya madini.
  • Kufanyia marekebisho sheria ya tasnia ya uziduaji (Uwazi na Uwajibikaji) Extractive Industries (Transparency and Accountability) ACT, 2015, Kufanya marekebisho kwa sheria ya Petroli namba 2 ya mwaka 2015 (Petroleum ACT, 2015 no. 2),  Kufanya marekebisho sheria ya usimamizi wa Mafuta na gesi (Tanzania Oil and Gas Revenue Management ACT, 2015). 
  • Serikali iweke mkazo kwenye usimamizi na utekelezaji wa maazimio ya Mpango wa EITI (Extractive Industries Transparency Initiative) ambapo nchi yetu ilijiunga na Mpango huu  mwaka 2009. EITI inazitaka nchi wanachama kuweka wazi mikataba, majina na taarifa za uchimbaji wa madini nchini na kuhakikisha rasilimali hizo zinatumika kusaidia ukuaji wa uchumi kwa maendeleo ya wote.
  • Serikali iharakishe zoezi la kununua mtambo wa kuchenjulia madini (smelter);
  • Serikali ifanye maamuzi sahihi katika masuala yanayogusa maslahi ya taifa ikiwemo uwazi na ushirikishwaji katika kuingia kwenye mikataba.
  • Kama sehemu ya matumizi bora ya rasilimali na kodi za wananchi, serikali itekeleze mapendekezo yanayotolewa na vyombo mbalimbali, asasi za kiraia, sekta binafsi nchini pamoja na ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.
  • Kuhakikisha uwiano sawa wa wanawake na wanaume katika nafasi za maamuzi kwenye vyombo vya maamuzi katika sekta ya madini ili kuleta ufanisi na kupunguza ubadhilifu.
  • Tunashauri kurejeshwa kwa mchakato wa Katiba mpya ili kuruhusu uwepo wa ibara zitakazolinda rasilimali zetu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

 

Imetolewa leo Juni 14, 2017 na

Lilian Liundi

Mkurugenzi Mtendaji

TGNP Mtandao