HATUA ALIYOCHUKUA MH. RAIS JOHN POMBE MAGUFULI JUU YA MAKONTENA YA MCHANGA WA MADINI (MAKINIKIA)

26 Mei 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

HATUA ALIYOCHUKUA MH. RAIS JOHN POMBE MAGUFULI JUU YA MAKONTENA YA MCHANGA WA MADINI (MAKINIKIA)

Sisi Wanamtandao wa Wanawake na Katiba/Uchaguzi na Uongozi tunatoa pongezi kwa serikali ya awamu ya tano kwa jitihada inayozionesha za kupambana na upotevu wa rasilimali za nchi, pia kwa kuonesha ujasiri wa kusimamia baadhi ya masuala yaliyokuwa yakipigiwa kelele kwa muda mrefu ikiwemo suala la ubadhirifu wa rasilimali za umma.

Taarifa ya Tume ya Rais ya Uchunguzi chini ya Prof. Mruma iliyowasilishwa Mei 24, 2017 iliyo kuwa inachunguza kiwango cha madini yaliyomo katika makontena 277 ya mchanga (Makinikia) yaliko katika Bandari ya Dar es Salaam na Bandari Kavu yaliyozuiliwa na serikali kusafirishwa kwenda nchi za nje. Ni ukweli kuwa kwa takribani miaka 17 viwango vya madini yaliyopo kwenye Makinikia havijulikani, na hata mikataba ya uchenjuaji haipo wazi.  Imebainisha kuwepo udanganyifu mkubwa kwenye kiwango cha madini yaliyopo kwenye mchanga na thamani halisi.

Katika makontena hayo, kwa kutumia viwango vya wastani thamani ya mtali/madini yote katika makinikia ni TZS bilioni 829.4 na TZS bilioni 1,438.8 kwa kutumia viwango vya juu. Na viwango hivi vya thamani havitumiki na kukadiria mapato ya serikali. Tunaungana na Tume kuwa huu ni upotevu mkubwa sana wa mapato kwa nchi yetu. Mahususi kwenye dhahabu taarifa za Wakala wa ukaguzi wa Madini (TMAA) zinaonyesha makontena haya yana tani 1.1 za dhahabu na thamani ya TZS bilioni 97.5 (USD 44,320,000), thamani hii ni ndogo ukilinganisha na thamani iliyopatikani kenye uchunguzi wa Tume ambao ni kati ya TZS bilioni 676 na TZS bilioni 1,147.

Ni dhahiri kuwa wananchi tumeibiwa sana kupitia usafirishaji wa makinikia nje ya nchi. Kwa mujibu wa taarifa hiyo Tanzania imekuwa ikipoteza kiasi cha takriban shilingi za kitanzania bilioni 744 kwa mwezi ambayo ni sawasawa na trilioni 9 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka 17. Kiasi hiki cha fedha zingeweza kuvunwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya taifa. Hatua iliyochukuliwa na Mh. Raisi John Pombe Magufuli ni hatua ya kijasiri na ishara nzuri na kwetu sisi, huu ni mwelekeo wa mafanikio ya kampeni yetu ya “Rudisha rasilimali kwa wananchi” na Haki ya Uchumi Rasilimali ziwanufaishe wanawake na wanaume walioko pembezoni” ambazo zimekuwa kwa muda mrefu na kubeba madai ya wananchi kuhusu rasilimali za nchi yao.

Tunatambua changamoto ya ulimwengu ni mgawanyo wa rasilimali kinyonyaji, na haya ndio matendo ya kinyonyaji yanayoendelea na mabepari Tanzania.

Ni jambo lisilopingika kwamba kumekuwa na changamoto kubwa katika upatikanaji wa huduma bora za jamii kama maji, elimu na afya ambapo mwanamke amekuwa muathirika mkubwa kwa ukosefu wa huduma hizi. Katika uchambuzi wa sera, mipango na bajeti ya taifa kwa mtazamo wa kijinsia inaonesha utengwaji wa kiasi kisichokidhi kuboresha upatikanaji wa huduma bora za jamii.

Kwa mwaka wa fedha 2016/17, utoaji wa fedha za bajeti ya taifa ya maendeleo; hadi kufikia mwezi Februari 2017 TZS. 3.9 trilioni kati ya TZS.11.3 trilioni za bajeti ya maendeleo sawa na 34% ya kilichopangwa kwa utekelezaji wa bajeti ya maendeleo ndio kimeweza kutolewa. Katika sekta mbalimbali hadi kufikia Machi 2017 ilikuwa kama ifuatavyo; sekta ya elimu ni 34%; maji na umwagiliaji 19.8%; Wizara ya afya maendeleo ya jamii, jinsia,wazee na watoto fungu la afya mpaka mwezi Machi lililotolewa ni 43%, fungu la maendeleo ya jamii , jinsia, wazee na watoto 26.7%; katika kilimo hadi mwezi Machi fedha za maendeleo ni 3% zilizoweza kutolewa ukifuatilia hii sekta mama ya kilimo takimu zinaonyesha mwenendo wake 2007/08 – 2016/17 kwa kipindi hicho imekuwa ni wastani wa 2.2% tu ya bajeti ya Taifa.

Utolewaji wa fedha kwa mwaka 2011/12 -2015/16 imekuwa wastani wa 57% ya fedha zilizoidhinishwa na kwa mwaka 2016/17 hadi mwezi Machi fedha za maendeleo zilitolewa asilimia 3% ya zilizoidhinishwa. Udhaifu huu wa utekelezaji wa bajeti ya maendeleo, pamoja na mambo mengine unachangiwa na; uhaba wa vyanzo vyetu vya ndani vya mapato lakini pia mianya mingi ya ukwepaji kodi na ulipaji stahiki nyingine za serikali ikiwemo ujanja wa baadhi ya wawekezaji kukwepa kulipa kodi.

Licha ya mazingira na misamaha ya kodi kisheria tuliyowapatia lakini bado tumendelea kudanganywa; makampuni mengi yamekuwa yakisema yamepata hasara na hivyo kutolipa kodi, wamekuwa wakihamisha mitaji, wanaficha mikataba na wamiliki na kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia kwa wananchi wanaozunguka migodi.

Ni dhahiri kuwa fedha hizi ambazo serikali imekuwa inazipoteza kwa miaka mingi ingeweza kuboresha hali ya huduma za jamii ikiwemo kuongeza vituo vya afya na zahanati, kuweka miundo mbinu ya maji na kuhakikisha maji yanapatikana, uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia ikiwemo vyoo, maji na mabweni hususan kwa watoto wa kike.

Sisi wanamtandao na wanaharakati wa haki za wanawake na makundi yalioko pembezoni, kwa kauli moja tunatoa mapendekezo haya:

 1. Tunaunga mkono mapendekezo ya Tume ya uchunguzi kama hatua za awali za kukabiliana na uporaji wa rasilimali zetu,
 2. Uchunguzi wa kina ufanyike ili kubainisha wale wote waliohusika wa njia moja au nyingine kushiriki kwenye uporaji wa rasilimali za taifa, mawaziri waliopita, makamishna na hata makatibu wakuu,
 3. Makampuni yote ya madini yachunguzwe ili kuhakiki uzingatiaji wa kulipa kodi,
 4. Makampuni yaliyohusika na uporaji huu yapelekwe kwenye mahakama za kimataifa. Na endapo watapatikana na makosa, wafidie uporaji waliokwisha fanya kwa miaka mingi,
 5. Mashine ya kuchuja yanunuliwe mara moja. Fedha znazokusudiwa kununua ndege zitumike kununua mashine hizo,
 6. Serikali iboreshe mifumo na sheria ili kuwezesha makusanyo sahihi ya mapato ikiwemo kodi na stahiki nyingine za serikali kutoka kwa wawekezaji,
 7. Serikali isimamie na kuhakikisha mamlaka zilizopewa dhamana ya kusimamia rasilimali za nchi zinafanya kazi kwa ueledi na ufanisi,
 8. Serikali ifanye maamuzi sahihi katika masuala yanayogusa maslahi ya taifa ikiwemo uwazi na ushirikishwaji katika kuingia kwenya mikataba badala ya kuachilia jukumu na mchakato mzima kwa kundi dogo la viongozi. Mikakati bunifu ya kuwezesha Wazalendo kushiriki kwa njia ya ubia ifanyike,
 9. Kama sehemu ya matumizi bora ya rasilimali na kodi za wananchi, serikali itekeleze mapendekezo yanayotolewa na vyombo mbalimbali inavyoviunda kwa gharama ikiwemo tume za uchunguzi, taasisi mbalimbali mfano ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.Serikali kupitia sheria zote za madini na mikataba ili kuzuia haya kutokea siku za usoni,
 10. Serikali kupitia sheria zote za madini na mikataba ili kuzuia haya kutokea siku za usoni
 11. Kutokana na mchakato huu kiasi kitakachopatikana kitumike kuboresha sekta zinazomgusa mwananchi wa kawaida hususan mwanamke na mtoto kwa kuboresha upatikanaji sekta ya huduma za jamii (elimu, afya na maji),
 12. Kuhakikisha uwiano sawa wa wanawake na wanume katika nafasi za maamuzi kwenye sekta ya madini ili kuleta ufanisi na kupunguza ubadhirifu.

Imetolewa na:

TGNP Mtandao

Kwa niaba ya; Women Fund Tanzania, Tanzania Women Lawyers Association, TAMWA, TWCP-ULINGO

Mwanamke Rafiki Original

TAWLA